Thursday 8 November 2012

Simu bandia Uganda kuzimwa 2013 ,habari njema kwa wamiliki simu za kichina

Uganda imeamua kusitisha mipango yake ya kuzima simu ghushi hadi tarehe moja mwezi Julai mwaka 2013.
Hatua ya serikali inayolenga kuzuia simu bandia kutumika katika mitandao ya simu nchini humo ilikuwa imepangiwa kuafikiwa mwishoni mwa mwezi huu.
Kenya iliweza kuchukua hatua sawia na hii mwezi Oktoba na kuzima simu za zaidi ya watu milioni moja.
Tume ya mawasiliano ya Uganda, imependekeza kuwa takriban asilimia kumi na tatu ya simu milioni kumi na saba za rununu Afrika Mashariki ni ghushi.
Watumiaji wa simu hizo, wana hadi mwezi Machi kuhakikisha kuwa kadi zao zimesajiliwa na tume hiyo.
Pia wametakiwa kubaini nambari yao ya kutambua simu ijulikanayo kama IMEI (International Mobile Equipment Identity) na ambayo huwa ipo kwenye simu halali. Simu ghushi kawaida huwa hazina nambari hii ya utambulisho.
Tume hiyo ya mawasiliano inasema kuwa hatua ya serikali itasaidia maafisa wa sheria kuwasaka wahalifu wanaotumia simu bandia.
Rwanda, Burundi na Tanzania ni miongoni mwa mataifa ya Afrika ambayo yamejadili mipango ya kuzima simu ghushi.
Simu bandia ni maarufu kwa sababu zina bei nafuu kuliko simu halali mara nyingi kwa sababu wanaoziuza huwa wamekwepa kulipa kodi.
Lakini maafisa wanasema kuwa zinaweza kusababisha athari kubwa za kiafya. Wanasema simu hizo hazijafanyiwa utafiti ikiwa ni salama .
Pia wameongeza kuwa simu hizo hazijatengezwa katika njia ambayo inaweza kutumika kwa mitandao ya simu,kwani zinaweza kusababisha simu kukatika mara kwa mara.

0 comments:

Post a Comment